Monday, January 15, 2018
KAMARI KAMALIZA
Kuna jambo nalikiri,maradhi yamesambaa
Ya wazi tena si siri,kote yanazua waa
Gonjwa hili nafikiri,metugeuza vichaa
Hili jambo la kamari,linakula halisazi
Wamejawa na ghururi,daima watuhadaa
Tena wapaka uturi,kamari ipate ng'aa
Kumbe ina takisiri,wanatuzulia baa
Hili jambo la kamari,linakula halisazi
Si uongo ni dhahiri,nyumba nyingi zina njaa
Darahima nafikiri,kamari zimezitwaa
Zilizobaki shubiri,moyoni zimetujaa
Hili jambo la kamari, linakula halisazi
Serikali tusitiri,iturejee shifaa
Maisha yawe ya kheri,ituondoke balaa
Makampuni maayari,waache kutuhadaa
Hili jambo la kamari, linakula halisazi
Nawapeni ushauri,jukuani nikipaa
Tuwaacheni kamari,tusigeuke vichaa
Kamari si takidiri,Mungu analikataa
Hili jambo la kamari, linakula halisazi
Subscribe to:
Posts (Atom)